WASILWA: Kibarua Cha Jaji Mkuu Mteule

WASILWA: Kibarua Cha Jaji Mkuu Mteule

“Utamu wa nyama ipikwapo hutegemea sana ukali wa mwanzo wa moto, mwanzoni moto ule unapofifia, nyama ile huenda ikakosa ladha iliyokusudiwa na mpishi”

Alipouliziwa hadhi ama kiwango cha ubora wa idara ya mahakama nchini, Nzamba Kitonga bila ya kupepesa macho alidokeza kuwa Idara ya mahakama ilikuwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi na sasa imo katika wadi za wagonjwa wa Kawaida. Jaji mkuu anayeondoka Willy Mutunga alinukuliwa wakati mmoja akisema, “uchumi wetu unaongoza na walaghai na pia idara ya mahakama imesheheni ufisadi”.

Hiyo ndio kadhia ya idara yetu ya mahakama.  Kwamba iwapo idara ya mahakama ingekuwa mwanadamu basi inafananishwa na mgonjwa ambaye sasa ana uwezo wa kula lakini hawezi akatembea mwenyewe lakini awali alikuwa mgonjwa asiye na matumaini. Idara ya mahakama ni moja kati ya tanzu tatu za serikali. Tanzu nyingine ni Urais na Bunge. Kikatiba tanzu hizo hazifai kushawisha na yeyote kwenye utenda kazi wao. Zote zinafaa kutekeleza majuku yao bila ya kuingilwa.

Kimsingi utenda kazi wao unastahili kuwa huru.  Kwamba baada ya mahojiano yaliyofanywa na Tume ya kuajiri watumishi kwenye idara ya mahakama, David Kenani Maraga,  ameibuka kidedea.  Jina lake limewasilishwa kwa rais ili kuidhinishwa kuwa Jaji mkuu mpya wa taifa a Kenya. Ni wazi kuwa Jaji Maraga ataapishwa kuwa jaji Mkuu wa 14 hivi karibuni tangu taifa lijinyakulie uhuru wake na wa pili chini ya katiba mpya. Kwamba alifurahisha Tume ya Idara za huduma wa mahakama.

Licha ya kuwa na watu wenye majina makubwa, Maraga alipata asilimia 84, Smokin Wanjala alizoa alama 74, Makau Mutua mwenye uzoefu wa sheria ya kimataifa aliridhika na nafasi ya tatu kwa alama 70, Nzamba Kitonga akawa wa nne, kisha Alnashir Visram akawa wa tano. Maraga alichaguliwa kwa sababu ya uadilifu, kujitolea kuleta mabadiliko na pia anaheshimiwa miongoni mwa wenzake. Maraga aliwaonyesha kivumbi watu wengine waliokuwa wakimezea mate kiti hicho kwenye mahojiano. Lakini David Kenani Maraga ni nani?

Jaji David Maraga Kenani alizaliwa miaka 64 iliyopita katika kijiji cha Bonyamatuta, Mugirango Magharibi katika kaunti ya Nyamira. Alisomea uanasheria katika chuo kikuu cha nairobi ambapo alipata shahada ya sheria na shahada ya uzamili katika masuala ya sheria. kabla ya kupata stashahada ama diploma ya sheria kwenye chuo cha mafunzo ya sheria ama kenya school of law mwaka 1978. Jaji Maraga alitawazwa kuwa jaji wa Mahakama Kuu mwaka 2003 ambapo alihudumu kwa miaka minane.

Aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa mwaka 2009 na kisha mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya Idara ya Mahakama. Jaji maraga ni muumini wa dhati ama kindaki ndaki wa kanisa la kisabato na kuwa imani hiyo ameipa kipau mbele si siri, kiasi cha kuwa hawezi kusikiza kesi siku ya Jumamosi. Anajieleza Kuwa mtu mwenye imani dhabiti tena mnyenyekevu na ayapenda kuzingatia saa kwenye utenda kazi wake. Licha ya kuwa ufahamu wake kwa umma huenda ukawa mdogo, Maraga anafahamika kwenye ushorobo wa mahakama kutokana na uzoefu wake katika masuala ya sheria kiasi cha maamuzi yake kutumiwa kama msingi katika kesi zisizopungua sabini na kadhalika kuundwa kwa sheria kuhusu mali katika ndoa.

Jaji Maraga alikuwa mwanasheria kwa miaka 25 kabla ya kutawazwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu. Wadhifa wa Jaji Mkuu ukiwa ndio upeo wa azma yake ya kikazi. Jaji Maraga anatambulika kwa wepesi wa kutoa maamuzi kiasi cha kuweza kukamilisha kesi 1000 katika mahakama ya rufaa ya kisumu katika kipindi cha mwaka mmoja pekee. Hata hivyo Wasifu kazi wa Maraga haukosi doa.

Akiwa Jaji wa Mahakama Kuu, alikosolewa kwa kumpunguzia hukumu afisa wa polisi aliyetuhumiwa kumuua aliyekuwa mbunge wa Ainamoi David Kimutai Too na kumwondolea hukumu ya kifo. Jaji Maraga alitoa hukumu ya miaka 10 tu, uamuzi alioshindwa kuutetea mbele ya Tume ya Kuwachunguza Majaji. Jaji Maraga ambaye aliponea msumeno wa Tume ya Sharad Rao ambapo alijitetea kutoshiriki ukabila na  ufisadi mwaka 2012 anaahidi kuondoa ufisadi mahakamani na kuunda jopo la majaji watatu na mchunguzi kutatua suala hilo.

Utenda kazi wake wa hivi karibuni ulikuwa kuongoza tume ya kumchunguza Jaji Mutava na kuamua kumpiga kalamu kwa ukosefu wa maadili kwenye utenda kazi wake. Amehudumu katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo Nairobi, Kisumu na Mombasa. Akiidhinishwa na Rais kuwa Jaji Mkuu, Jaji Maraga anapania kupigania kuongezwa kwa muda wa kusikiza kesi za uchaguzi wa urais kutoka siku 14 hadi 30.

Jaji anayeondoka Willy Mutunga amekuwa na panda shuka za hapa na pale. Ila mgaala muue na haki umpe. Mutunga atakumbukwa kwa kupigania uhuru wa idara hiyo, kuimarisha imani ya wakenya kuhusu idara hiyo. Aidha kwenye uongozi wake idadi ya majaji iliongezwa kutoka 53 hadi 143. Mutunga ameacha korti 17 mpya katika maeneo kama vile Garissa, Marsabit na Garsen kuleta huduma hiyo karibu na wananchi.  Aidha Mutunga  ameacha Mahakama za Rufaa katika maeneo ya Kisumu Nyeri na Malindi.

Iwapo rais atamuidhinisha, Maraga atakuwa Jaji Mkuu wa pili nchini ya katiba mpya. Wakenya wana matarajio makubwa kwake.  Ana kibarua kigumu cha kubadilisha idara ya Mahakama, kukabili saratani ya ufisadi ambayo imekolea kwenye ushoroba wa Mahakama. Aidha kuna rundo la kesi ambazo zimekusanya vumbi kwa miaka na mikaka. Inasemekana kuwa kuna yamkini kesi 500,000 ambazo zinasubiri kuamuliwa.

Mzigo mzito ambao atakuwa nao iwapo utakuwepo ni uamuzi wa kesi ya urais kwenye uchaguzi mkuu ujao. Hapo atahitajika kuwa na hekima ya Mfalme Suleimani. Atoe uamuzi ambao hautakwaza upande wowote wa siasa. Afahamu fika kuwa uchaguzi mkuu ujao una matarajio mengi kwa mirengo mbali mbali ya siasa na Wakenya, kosa dogo tu la uamuzi litatumbukiza taifa kwenye lindi na jangwa la vurugu. Kwenye mahojiano na tume ya huduma za mahakama, Maraga alijitokeza kuwa mcha Mungu, kwenye utenda kazi wake, kila mara wakenya watakuwa wanamkumbusha hulka na silka hiyo.

Amebeba sio matumaini ya Wasabato bali wakenya wote. Huku Majaji wakitakiwa kustaafu wakiwa na miaka 70, Jaji Maraga atahudumu kwa kipindi cha miaka sita na kisha kustaafu. Kwamba kiti atakachokalia sio baridi ni moto. Amebeba matumai ya Wakenya milioni 40.  Kiti hicho kina mawimbi yanayoitwa ukabila, kina upepo unaoitwa ufisadi, na pia kina mamba na papa wanaoitwa maadui wa ustawi. Kumudu changamoto hizo anastahili kuwa tayari kwa lolote, kwani hii ni Kenya yetu.  Kwa Jaji Maraga hicho si kibarua chepesi. Atahitaji bidii za mchwa, werevu wa nyoka, moyo wa simba na upole wa njiwa na wakati mwingine ukaidi wa mbuzi ili kufanikisha utenda kazi wake. Moto atakaonza nao Maraga utachangia mwisho wa nyama iliyoiva na kuwa na ladha inayokusudiwa na kutarajiwa na Wakenya.

Shisia Wasilwa ni mhariri wa Citizen Nipashe

Maoni haya hayana uhusiano wowote na msimamo wa Royal Media Services Ltd.

latest stories