JAMILA'S MEMO: Tusikilizane, ama?
On my memo, allow me to use the language that is most used in political rallies… sijui kama tumeelewana… from now on, it’s Kiswahili.
Wakati wa kampeni,
ahadi chungu nzima hutolewa. Tutatenga, tutapanga, tutatimiza ni matamshi
ambayo hutolewa sana wakati huo.
Kuna sababu tofauti za kuchagua viongozi hapa nchini Kenya: kabila la kiongozi huyo, chama chake cha kisiasa, ama eneo analotoka.
Lakini sababu muhimu zaidi ni ahadi zinazotolewa. Wananchi wakiwa na matumaini yatatimizwa iwapo viongozi wanaotoa ahadi hizo watachaguliwa.
Ila kuna changamoto kubwa
ambayo hujitokeza punde tu uchaguzi unapokamilika; ahadi inapuuzwa. Hakuna
mipango ya kuzitimiza—yaani mambo yalikwishia katika kuweka ahadi wakati wa
kampeni. Hakuna plan baadaye.
Na ahadi zisipotimizwa
mara ya kwanza, watu wanaambiwa tupeni muda zaidi, tutatimiza. Tulipata mambo
yakiwa mabaya sana. Itatuchukua muda kuyarekebisha. Watu wanatulia tena. Ahadi
zingine zinavunjwa, hakuna maelezo yanayotolewa. Ila baada ya muda,
inadhihirika kuwa hizi zilikuwa tu story za jaba.
Na muda unavyoendelea
kuyoyoma, athari za ahadi kutotimizwa zinaanza kudhihirika. Wananchi wanachoka
kusikia maneno yale yale ambayo yanaanza kupoteza maana. Na maneno ya kiongozi
yanapoanza kutodhaminiwa, ni ishara ya hatari kubwa.
Sauti za minung’uniko
ya wananchi zinaanza kusikika. Walioko uongozini wanaona hawa ni wachache,
tuwapuuze. Ni kelele za chura.
Lakini baada ya muda,
wachache wanakuwa wengi. Na kisha sauti za minung’uniko zinaendelea kuongezeka
na kupazwa zaidi. Wanaozungumza ni watu tofauti—wakubwa kwa wadogo—wanaotoka sekta
mbali mbali. Sauti ni tofauti lakini ujumbe ni ule ule: tunachoshwa na jinsi
mambo yanavyoendeshwa, tunachoshwa sana. Hali yetu ilikuwa bora awali, ila sasa
ni kuhangaika.
Ila wanaendelea
kupuuzwa na viongozi. Miradi mipya inazinduliwa. Hakuna maelezo kuhusu
ilikotoka miradi hii na kwanini inazinduliwa. Itamfaidi nani? Mara nyingi
maelezo ni fiche, hayaelezwi kwa umma. Wananchi hao wanatarajiwa kukubali tu na
kunyamaza. Wanaambiwa kelele zenu za kukataa kila kitu zimezidi.
Wakati mwingine
yanayozinduliwa yananuiwa kutatua tatizo ambalo sio la dharura, ama ukipenda it’s
not a priority. Kwa Kiingereza wanasema if it ain’t broken, why fix it?
Maswala ambayo yanahitaji kuangaziwa ni mengi sana. Mbona hakuna juhudi
zinazoelekezwa huko?
Iwapo mfumo wa afya
uliokuwa unatumika kwa muda mrefu ulikuwa na kasoro fulani, tatua hiyo. Na
iwapo mfumo wa malipo ya masomo ya vyuo vikuu uliokuwa ukitumika ulikuwa na
changamoto za hapa na pale, zitatuliwe. Sio kubadilisha kila kitu. Ama iwapo
kuna mabadiliko, yafanywe kwa taratibu na kupewa muda wa kutosha, sio kuamka tu
na kusema tunabadilisha—mpende msipende.
Uongozi sio wa kila
mtu. Kuchukua majukumu ya uongozi ni jambo kubwa sana. Na ni muhimu kama
kiongozi uwe unafikiria uzito wa majukumu hayo. Kuna watu wanaokuangalia wakitarajia
utabadilisha maisha yao.
Muda wa uongozi sio
mrefu. Wanaochaguliwa wana muda mfupi sana kufanya kazi, kuwahudumia
waliowachagua, kuleta mabadiliko na kutimiza ahadi. Lakini iwapo muda
unapotezwa, ahadi zinavunjwa na wananchi wanaonekana kupuuzwa, kuna hatari
kubwa.
Ama ni sisi wananchi
ambao tunachagua viongozi kwa sababu katiba inatupasa kufanya hivyo, na sio kwa
sababu tunawachagua kuleta mabadiliko. Wakuje wamalize muda wao, waondoke,
kisha tuchague wengine kipindi kingine cha uchaguzi kitakapowadia… and the
cycle continues.
Want to send us a story? SMS to 25170 or WhatsApp 0743570000 or Submit on Citizen Digital or email wananchi@royalmedia.co.ke
Comments
No comments yet.
Leave a Comment