WASILWA: Nyota ya Ali Hassan Joho

WASILWA: Nyota ya Ali Hassan Joho

Kila kizazi huwa na nyota wake, mtu ambaye ni jasiri, shupavu asiye na uwoga na zaidi ya yote huangaza kwenye kundi la makumi ya maelfu. Hata hivyo mara nyingi, changamoto kwenye maisha yake hutisha kufumba nyota yake, mwanzo wake ukawa hafifu.  Kwamba jamii hukusa kuona uwezo wake, ndio maana kwenye Biblia takatifu, Yesu akawaambia wenyeji wa Nazareti kuwa nabii hana heshima kwao. Mwana wa seremala atatuambia nini naye. Maanake walimuona mazingira alimokulia, hakuwa tofauti nao,ila hawakuwa na ufahamu alikuwa ni nani hasa.

Mtu ambaye nyota yake imesimama katika jamii, anapojitokeza kwenye hafla na mikutano ya hadhara, wala huwa hasumbuki kutafuta maneno, anaposema maneno yake hukata na kuingia kwenye masikio mazito ya wale anaowahutubia. Watu wakaajabia uwezo wake wa uongozi pamoja na haiba yake. Kimsingi huwa hajilazimishi kwa watu. Ni mwepesi wa kushawishi umma upande wake. Huyu ni mtu ambaye kila mrengo wa siasa hutaka kuwa naye upande wake. Watu hawa si lazima wawe wanasiasa. Huenda nyota zao zikaangaza kwenye njanya nyingine za jamii kama vile elimu, tiba, biashara, sheria na kadhalika.

Kwenye medani ya siasa nani hatambui ushupavu wa hayati Jaramogi Oginga Odinga? Josiah Kariuki maarufu JM Kariuki, Masinde Muliro, Martini Shikuku mwana wa Oyondi, Robert Ouko, Alexender Muge? Marekani walikuwa na Martin Luther King, Tanzania walikuwa na hayati mwalimu Kambarage Nyerere, Nigeria walikuwa na Nnamdi Azikiwe. Na je, naibu Rais William Ruto?

Ruto hakurithi utawala wa siasa za eneo la Bonde la Ufa. Rais mstaafu, Daniel arap Moi, hakumkabidhi utawala. Kwamba alipotwaa usukani na kuwa msemaji wa jamii ya Kalenjin, pengo kati yake na rais mstaafu aliyemfunza siasa hakumuonea raha. Leo unapotaka kiti chochote cha kisiasa kwenye eneo  hilo, lazima utafute usuhuba na Ruto.

Nani hafahamu kinara wa upinzani Raila Amollo Odinga? Raila Amollo Odinga ni kimbunga kwenye siasa za taifa na nje ya nchi. Umpende ama umchukie mchango wake kwenye uga wa siasa za taifa hauna mipaka. Ila leo tunaagazia nyota ya Ali Hassan Joho, Gavana wa Mombasa.  Je, mwana huyu wa Pwani atahimili mawimbi ya siasa yanayotisha kufisha nyota yake baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2017?

Ali Hassan Joho ni mzawa wa Mombasa mwaka 1976, alijitosa kwenye siasa mwaka 2004, na kuwa mwenyekiti wa chama cha Liberal Democratic kati ya mwaka 2006-2007.  Kwenye uchaguzi mkuu uliondaliwa mwaka 2007 alichaguliwa na wakazi wa Kisauni kwa wingi wa kura kuwaakilisha kwenye bunge kwa tiketi ya chama cha ODM.

Kwenye serikali ya mkate nusu alichaguliwa kuwa waziri msaidizi kwenye wa uchukuzi. Machi nne mwaka 2013, alichaguliwa kuwa Gavana wa Mombasa. Gavana wa Mombasa, si mtu wa kupepesa maneno yake. Ukimkata, damu yake ni ODM. Anaamini kuwa jamii za pwani zilipigia kura chama hicho kwenye uchaguzi wa mwaka 2007 na mwaka 2013 kwa sababu ziliona kuwa chama hicho kiliipa kipau mbele mfumo wa ugatuzi.

Kisiasa Joho, ni mtu ambaye anakwea vidato. Tangu mwaka uanze, Joho ametia juhudi kuvutia na pia kujenga nafasi ya kuwa mfalme wa siasa za Pwani. Ametangaza kuwania urais mwaka 2022. Iwapo atahalisi ndoto yake atakuwa mwanasiasa wa tantu kutoka kwenye maji ya chumvi kufanya hivyo. Wengine wawili walikuwa Ronald Ngala mwaka 1963 na daktari  Chibule wa Tsuma, mbunge wa zamani wa Kaloleni mwaka 2002. Ni kwa nini nyota ya Joho inazidi kungaa?

Mapema mwaka huu, Gavana Joho aliwakosoa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kuhusu suala tata la maskwota kwenye ardhi ya waitiki. Joho alikosoa serikali kwa kuwatoza maskwota hela ili kuweza kuwapa ardhi hiyo. Joho pia aliteta kwa kuachwa nje ya ratiba ya Rais alipozuru Mombasa na akatangaza kuwa chama chake ni cha ODM na kwamba hataondoka.

Hatua hiyo ilichora taswira ya kiongozi asiyeogopa kupigania haki za watu wake, kiongozi asiyeogopa mtu yeyote na kiongozi anayesimamia ukweli licha ya athari. Joho ameonyesha kuwa hategemei mtu yeyote kupata umaarufu ama kumpa uongozi. Ni kiongozi ambaye anajitafutia, hajatulia kwenye kiti kupewa uongozi.

Jambo la pili ambalo limechochea kupaa kwa umaarufu wa Joho, ulikuwa  ushindi wa chama cha ODM kwenye uchaguzi mdogo wa Malindi. Japo ulitia msumari moto kwenye uhusiano kati yake na serikali ya kitaifa, lakini ukamwongezea umaarufu katika eneo la Pwani. Ushindi huo ukawa pigo kwa hasimu wake mkuu wa siasa ambaye ni Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Gideon Mungaro. Kuondolewa kwa Mungaro kuwa mwenyekiti wa wabunge wa Pwani kumemwongeza Joho hadhi ya ufalme kwenye siasa za Pwani. Kwamba si mdahalo kuwa kati ya magava sita wa Pwnai, Joho ndiye anasimamia kaunti ya pili kwenye ushawishi nchini kisiasa na kiuchumi.

Uzito wa Mombasa umetajwa kuwa, inapokohoa, pwani mzima hupata mafua na kichefuchefu. Kwamba Joho si tu Gavana wa Mombasa bali pia ni naibu mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha ODM. Ndiye kigogo na uzi unaounganisha chama hicho na Pwani mzima. Joho ndiye chanzo cha Mawimbi ya ODM yaliyofagia na kutanda Pwani mzima kwenye chaguzi za mwaka 2007 na mwaka 2013.

Iwapo Joho atasalia kuwa mwenye subira na mwaminifu wa Raila Amollo Odinga wadadisi wanasema kuwa huenda akatoshea kwa urahisi kwenye vyatu vya kiongozi wake wa chama na hata kumrithi. Unapotazama, viongozi kutoka pembe zote kwenye chama cha ODM, Joho anawabwaga wote. Kwamba amefanyia  chama cha ODM mengi si mdahalo.

Hata hivyo ni muhimu kumkumbusha Joho kuwa siku zote simba mwenda pole ndiye mla nyama. Na kwamba taratibu za kobe zilimfikisha mbali na salama. Lakini kwa Joho kufaulisha ndoto zake za mwaka 2022, lazima akabili upepo unaotisha kwenye kinyume chake uchaguzi mkuu uajo unapokarbia. Katika kaunti ya Mombasa, uongozi wake unakabiliwa na changamoto ndani na nje ya Mombasa.

Mkosoaji wake mkuu ni Senata Hassan Omar ambaye ametangaza kuwania kiti cha Ugavana kwenye uchaguzi mkuu ujao. Kiunzi kingine kwa safari ya Joho ni Mbunge wa Nyali Hezron Awiti Bollo ambaye pia na ndoto za kuwa Gavana wa Mombasa mwaka 2017. Anamkosoa Joho kwa utenda kazi duni wake. Licha ya changamoto hizo na udhaifu wake, Joho ana nafasi ya kuingia kwenye mabuku ya historia kama vile Ronald Ngala, Karisa Maitha na Sharrif Nassir.

Ili kufanikisha azma yake, Joho lazima avue gamba kwamba yeye ni mwanasiasa wa Pwani ili apate uungwaji mkono na Wakenya wote. Lazima ajitahidi kujaza lile pengo. Litakuwa jambo la busara kuanza kuzunguka Kenya nzima mapema kujifahamisha na jamii zote. Kwamba kila mara anapoonekana kwenye hafla za chama cha ODM, Joho huleta upya wa aina Fulani sio mdahalo.

Ila safari ingali ndefu kwake. Kwa sasa ubichi wa ujana uko upande wake pamoja na kwamba ana raslimali za kutosha kiasi cha kujipiga kifua kwamba hawezi akanunuliwa, ni bayana kuwa ni mmoja wa wanasiasa ambao darubini itakuwa inawafuata kwa karibu sana kwenye uchaguzi na baadaye. Kimsingi mustakabali wake ni pevu na wenye matumaini.

Kwenye kitabu cha Robert Green, maarufu 48 Laws of Power, anahoji kuwa: “Mamlaka ni mchezo na kwenye mchezo huwezi ukatao ukawahukumu mahasimu wako kwa kuzingatia nia zao bali kwa athari za matendo yao.”

 Shisia Wasilwa ni mhariri wa Ctizen TV

Makala haya hayahusiani na msimamo wa Royal Media Services Ltd. 

Want to send us a story? Submit on Wananchi Reporting on the Citizen Digital App or Send an email to wananchi@royalmedia.co.ke or Send an SMS to 25170 or WhatsApp on 0743570000

Leave a Comment

Comments

No comments yet.

latest stories