Narok: Wanafunzi 31 wakosa kufanya mtihani wa KCPE

Imebainika watahiniwa 31 waliosajiliwa kufanya mtihani wa KCPE katika shule kadhaa eneo bunge la Narok mashariki hawajajitokeza kufanya mtihani.

Kamishna wa Narok George Natembeya anasema baadhi wamekosa kufanya mtihani kwa sababu ya mimba na ndoa za mapema huku wengine wakisemekana kutoweka pindi tu walipojisajili kwa mtihani huo.

Kamishna huyo anasema kwamba eneo bunge hilo limekuwa likikumbwa na changamoto za mimba na ndoa za mapema, hali ambayo inaendelea kuathiri pakubwa elimu ya mtoto wa kike katika eneo hilo.

Baadhi ya shule zilizoathirika ni pamoja na shule ya msingi ya Olasiti Township ambapo watahiniwa 5 hawajajitokeza kufanya mtihani huo, Olenkomeei ambapo watahiniwa 3 hawakujitokeza, Ilkirragarien watatu, Nkinye wanafunzi wawili miongoni mwa shule zingine.