Mapigano Marsabit: Watu 8 wauawa, zaidi ya nyumba 100 zateketezwa

Mapigano Marsabit: Watu 8 wauawa, zaidi ya nyumba 100 zateketezwa

Shule moja imefungwa na zaidi ya nyumba mia moja kuteketezwa huku idadi ya waliouawa kwenye mapigano ya kijamii katika kaunti ya Marsabit ikifikia nane.

Hali ya taharuki kwa sasa imetanda katika vijiji vya Hurr na Qubi Qallo ambako mapigano hayo yameripotiwa.

Watu wanne waliuawa katika makabiliano ya kulipiza kisasi kati ya jamii mbili kijijini Qubi Qallo.

Mapigano hayo yalianzia katika kijiji cha Shurr ambapo watu watatu na mvamizi mmoja waliuawa wiki iliyopita.

Hapo jana makabiliano makali yalipelekea watu zaidi ya 350 kuathirika huku nyumba zao zikichomwa.

Kufuatia makabiliano hayo, shule moja imefungwa huku watoto wakikimbilia usalama wao pamoja na wazazi wao. Mifugo pia waliibwa wakati wa shambulio hilo.

Wasimamizi wakuu wa usalama Marsabit wamesema kuwa maafisa wa usalama wanashika doria katika maeneo yalioathirika.

Kwa sasa operesheni ya kutafuta mifugo walioibwa inaendelea huku ikidaiwa kuwa mifugo hao bado hawajahamishwa nchi jirani ya Ethiopia.

Wakati huo huo viongozi wa kidini wamelaumu wanasiasa katika kaunti hiyo kwa mauaji hayo huku wakidaiwa kuanzisha uchochezi na kisha kutotuliza ghadhabu za wakaazi.

Mwezi uliopita inspekta mkuu wa Joseph Boinnet, alizuru kaunti hiyo na kuonya dhidi ya mashambulizi baina ya watu wa jamii hizo mbili. Boinett aliwataka wanasiasa wanaochochea uhasama wakamatwe.